Milipuko yatikisa mji wa Kano, Nigeria

Mji wa Kano Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Milipuko ilitokea katika mji wa Kano

Watu kadhaa wameripotiwa kuuawa kwenye milipuko iliyotokea katika mji wa Kano, kaskazini mwa Nigeria.

Vituo vya Polisi pamoja na makao makuu ya Polisi eneo hilo ni miongoni mwa sehemu zilizolengwa katika mashambulizi hayo.

Milio ya risasi pia imesikika katika sehemu kadhaa.

Kundi la kiislamu la Boko Haram limesema ndilo lililotekeleza mashambulizi hayo.

Kundi hilo ndilo limekuwa likiendesha ghasia katika siku za hivi karibuni, kwenye eneo la kaskazini mwa Nigeria, lililo na Waislamu wengi.

Utawala katika jimbo la Kano umetangaza amri ya kutotoka nje ya muda wa saa 24.

Walioshuhudia walisema watu wawili waliuawa.

Lakini taarifa zingine ambazo hazikuthibitishwa zilisema idadi ya waliokufa ni kubwa zaidi.

Mwandishi wa BBC mjini Kano anasema kulikuwa na vurumai katika mji, huku moshi mkubwa ukitanda angani.

Mwandishi wetu anasema mbali na makao makuu ya Polisi yaliyoko magharibi mwa mji huo, vituo vingine vya Polisi kwenye eneo la katikati na kusini vililengwa.

Pia ufyataulianaji wa risasi uliripotiwa kwenye jengo muhimu la Polisi mashariki mwa mji.

Mkazi mmoja karibu na mji huo aliambia BBC kwamba aliona miili ikibebwa kutoka kituo cha Polisi karibu na eneo la kati kati mwa mji, lakini hakujua watu hao walikuwa wamekufa au kujeruhiwa.

Walioshuhudia walisema mlipuaji aliyeshambulia makao makuu ya Polisi alikaribia jengo hilo akiendesha pikipiki, akashuka na kukimbia ndani ya jengo akibeba mfuko.

Mlipuko mwingine ulikuwa katika afisi ya kutoa paspoti ya Kano.

Boko Haram limekiri kuhusika pia.

Msemaji wa kundi hilo Abul Qaqa, aliambia BBC akiwa kaskazini mwa mji wa Maiduguri ambao ndio ngome yao kwamba walitekeleza mashambulizi hayo kwa sababu serikali imekataa kuwaachia huru wafuasi waliokamatwa mjini Kano.

Kundi hilo linataka kuwepo utawala wa Kiislamu nchini Nigeria.

Lilianzisha ghasia mwaka 2010 mjini Maiduguri, zaidi likilenga taasisi za serikali.

Wadadisi wanasema shambulio la Ijumaa ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutekelezwa na Boko Haram, na kubwa zaidi mjini Kano.