Naibu kiongozi wa Libya ajiuzulu

Naibu kiongozi wa serikali ya mpito ya Libya amesema kuwa anajiuzulu, huku maandamano ya kumpinga yakizidi kufanywa katika mji wa Benghazi, mji wa pili kwa ukubwa.

Haki miliki ya picha AFP

Abdel Hafiz Ghoga aliiambia Al Jazeera, kwamba anajiuzulu kwa sababu ya masilahi ya taifa.

Hapo jana, waandamanaji mia kadha walivamia makao makuu ya serikali ya mpito mjini Benghazi.

Mabomu kadha yalirushwa.

Bwana Ghoga -- ambaye piya ni msemaji wa serikali - amelengwa, katika madai ya kutaka serikali ya mpito kuwa na uwazi zaidi.

Baada ya karibu majuma mawili ya maandamano mjini Benghazi, serikali ya mpito, inataraji kuwa kujiuzulu kwa naibu huyo, kutapunguza chagizo.

Abdelhafiz Ghoga ndiye aliyelengwa na hasira.

Baadhi ya waandamanaji wanamshutumu kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na serikali iliyopita, ya Gaddafi.

Wanamuelezea kuwa na nyuso kadha.

Lakini madai yao yanafika mbali zaidi.

Wanataka serikali ya Libya iwe na uwazi zaidi jinsi inavotengeneza sheria mpya, na jinsi inavotumia fedha za taifa.

Waandamanaji wengi wamepoteza jamaa, marafiki, au viungo katika vita vya miezi 9 dhidi ya Kanali Gaddafi.

Sasa wanadai nao wawe na mchango katika hatima ya nchi hiyo.