Wafuasi wa Boko Haram wakamatwa

Polisi wawasaka  Boko Haram mjini Kano Haki miliki ya picha google

Kikosi maalum la kijeshi lililobuniwa nchini Nigeria limefanikiwa kuwatia mbaroni washukiwa mia moja hamsini na nane wa kundi la wanamgambo wa kiislamu wa Boko Haram katika mji wa Kano, siku tatu baada ya watu mia moja themanini na watano kuuwawa na wanamgambo wa kundi hilo.

Watu wasiopungua wawili waliuwawa katika kamata kamata hiyo ya jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram.

Kuna ripoti kwamba shambulio jingine dhidi ya kituo cha polisi katika mji wa Kano limetekelezwa hapo jana jumanne, haya ni kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Kikosi cha jeshi la Nigeria na police maalum waliopewa jukumu la kupambana na Boko Haram wamewakamata washukiwa 158 wa kundi hilo katika msako wa huko eneo la Kano.

Hata hivyo wakaazi wasema mtu na mkewe mja mzito wameuawa katika oparasheni hiyo.

Rais Goodluck Jonathana ameapa kutokomeza kundi hilo lililofanya mashambulio,la hivi punde likiwa lile la siku ya ijumaa huko Kano ambapo walisababisha vifo vya watu 185 wakiwemo polisi na maafisa wa idara ya uhamiaji.

Boko haram walishambulia baada ya dola kukataa kuwaachia huru wana-boko haram wengine waliokuwa wamekamatwa.

Itakumbukwa jinsi mshukiwa mmoja mkuu katika shambulio lilofanywa wakati wa krismas , alivyotoroka kutoka kizuizi cha polisi hapo mapema mwezi huu.

Mashambulio ya Boko haram yamesababisha vifo vya karibu watu elfu moja katika kipindi cha mwaka mmoja sasa.