Maadhimisho Misri baada ya mwaka mmoja

Medani ya Tahrir Haki miliki ya picha Getty
Image caption Maadhimisho ya Wamisri katika medani ya Tahrir

Maelfu ya wananchi wa Misri wamekusanyika katika Medani Tahrir mjini Cairo kuadhimisha mwaka mmoja ya mapinduzi yaliyomng'oa madarakani Rais Hosni Mubarak.

Baadhi yao wanasherehekea mafanikio ya vyama vya kiislamu katika uchaguzi wa kwanza baada ya kuondoka kwa Mubarak;huku wengine wakihimiza mageuzi zaidi ya kisiasa.

Sheria za hali ya hatari ambazo zimetumika kwa muongo mzima zimeondolewa ili kuadhimisha siku hiyo.

Bw Mubarak anakabiliwa na mashtaka ya kuamuru waandamanaji wauwawe madai ambayo anayakanusha.

Mamia ya watu waliohukumiwa adhabu ya vifungo jela na mahakama za kijeshi walitazamiwa kuachiliwa siku ya jumaatano katika hatua inayodhaniwa ya kuwaridhisha waaandamanaji.

Usiku wa Jumaanne maelfu ya watu walipiga kambi katika medani ya Tahrir,nembo ya maandamano ya mwaka jana wakiungwa mkono baadaye na maelfu wengine wakiwakilisha mirengo mipya ya siasa za kiislamu na za wastani.

Mwaandishi wa BBC Jon Leyne, akiwa mjini Cairo, anasema hali imekua ya utulivu hadi sasa ikionekena kama ni karamu kubwa mitaani badala ya maandamano ya kisiasa.