Afrika yashikilia uzi wake Davos

Kikwete
Image caption Rais Kikwete ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria

Mji wa Davos, Uswizi, wakati huu wa kipupwe Ulaya, huwa baraza la domo kaya. ‘Wakuu’ kutoka nyanja mbalimbali za biashara, kisiasa, kisomi na viongozi wengine wa kijamii hujumuika kuongelea jinsi ya kunyanyua ajenda za kieneo na tasnia duniani.

Ingawaje, samli kwa mwenye ng’ombe. Viongozi kutoka nchi kadha za Afrika wiki hii wamefika Davos kutoa mchango wao.

Viongozi wa Afrika mjini Davos wameshikilia uzi mmoja, ushirikiano wa karibu zaidi barani kuhusu nishati na miradi ya miundo-mbinu, kwa kukuza maendeleo ya Afrika.

Wakishiriki katika kikao chini ya mada “Afrika: toka Mpito hadi Mgeuzo”.

Miongoni mwa viongozi hao ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania. Mojapo ya vikwazo vikubwa kwa maendeleo katika Afrika, alisema, ni tatizo la ufisadi na dawa “ni uangavu”.

Ni kwa sababu hiyo Tanzania sasa huchapisha kandarasi zote za uchimbaji maadini kama sehemu ya kanuni mpya za machimbo.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema Waafrika lazima wafanye biashara baina yao, ambayo Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, aliieleza kama ni ‘ndogo sana’ kinyume na nchi za Ulaya ambazo hufanya zaidi biashara kati yao kuliko sehemu nyengine za dunia.

Na Rais Alpha Conde wa Guinea-Conakry alitoa wito viongozi wa Afrika, wakome kuweka pesa zao benki za ng’ambo na kuendeleza rasilimali kwa manufaa ya watu wao wenyewe.

Pia viongozi waache ubinafsi, “kupigania madaraka badala ya kupigania watu wetu”, alisema.

Mwenyekiti wa kikao kuihusu Afrika, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown, alisema, Afrika inahitaji uwekezaji wa mabilioni ya dola katika miundo-mbinu, lakini utawala-msonge na matatizo ya uvukaji mipakani yanatatanisha.

Rais Zuma alisema matatizo hayo - mipaka wazi, upitaji huria wa watu, wafanyakazi, na bidhaa, pamoja na uwekezaji - yanavaliwa njuga.