Shinikizo dhidi ya Syria laongezeka

Waandamanaji nchini Syria Haki miliki ya picha BBC World Service

Mataifa ya magharibi yanajiandaa kupigia debe azimio kali kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro uliopo nchini Syria.

Katibu mkuu wa muungano wa Mataifa ya Kiarabu Nabil al-Arabi anatarajiwa kutoa ombi kwa Baraza la Usalama kuunga mkono mpango mpya wa muungano huo unaotaka rais wa Syria Bashar al-Assad ajiuzulu.

Mawaziri wa mashauri ya nchi za kigeni kutoka mataifa ya magharibi wanaounga mkono mpango huo wa muungano wa Mataifa ya Kiarabu watajaribu kuzuia tishio la Urusi kupiga kura ya turufu dhidi ya azimio hilo.

Afisa mmoja kutoka wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Syria amesema kuwa Syria 'itashinda sera za kuzua vurugu', shirika la habari linalomilikiwa na serikali Sana limesema.

"Tunasikitika kwamba matamshi kama hayo bado yanatolewa na mataifa yaliyo na mazoea ya kufanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa uwanja wa kuonyesha upumbavu wao pamoja na majaribio yao yasioleta manufaa," afisa huyo akaongeza.

Mpango huo uliopendekeza na muungano wa nchi za Kiarabu na kuungwa mkono na Marekani, Uingereza na Ufaransa, unaotoa wito kwa Bw. Assad kukabidhi madaraka kwa naibu wake ambaye ataunda serikali ya muungano wa kitaifa.

Moscow imesema kuwa mpango huo "hauna usawa" na "utatoa mwanya'' wa uingiliaji wa maswala ya ndani ya Syria.

Ikulu ya White House ilisema Jumatatu kwamba bwana Assad alikuwa ameshindwa kuidhibiti Sria na kuongeza kuwa sharti ''ataondoka''

Marekani imetoa wito kwa mataifa yote kutoa msimamo wao kuhusiana na kile ilichokitaja kuwa udhalimu serikali ya Syria.