Serikali yafuta Chama cha mpira Misri

Nchini Misri Waandamanaji wamerejea katika mitaa ya mji mkuu Cairo kuonyesha hasira yao juu ya maisha yaliyotokomea jana kwenye mashindano ya mchezo wa mpira wa miguu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waomboleza vifo vya uwanja wa mpira

Watu sabini na wanne walipoteza maisha yao katika uwanja wa mpira ulio katika mji wa kaskazini mashariki wa Port Said.Mamiya wengine walijeruhiwa.

Kwenye kikao cha dharura cha bunge, Waziri mkuu wa nchi hio ametangaza kua wanakamati wa Chama cha mpira cha nchi hio wote wamefutwa kazi na wanachunguzwa. Gavana wa mji wa Port Said amejiuzulu.

Waziri Mkuu wa Misri Kamal Ganzouri ametangaza hatua ya kuwafuta kazi wanachama wote wa chama cha mpira cha Misri na kujizulu kwa baadhi yao kwenye Kikao cha dharura cha Bunge.

Hatua hio hata hivyo huenda isitoshe kuwaridhisha Wamisri wengi. Kuna dalili la kuongezeka kwa ghadhabu ya wa Misri juu ya Wizara ya mashauri ya nchini inayosimamia Polisi, ambayo wengi wanahisi haijabadilika tangu enzi za Hosni Mubarak.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Field Marshall Tantawi

Na ghadhabu hizo zimemuelekea kiongozi wa Misri wa kijeshi Field Marshall Tantawi. Mashabiki wa klabu ya Al Ahli, ambao wenzao walishambuliwa mjini Port Said, wameanza safari ya miguu kuelekea medani ya Tahrir na makao ya Wizara ya masuala ya ndani.

Wabunge kutoka chama cha Muslim Brotherhood wanaongoza katika kuikashifu serikali bungeni. Kila mmoja anahofia kua huenda haya yakazua duru mpya ya malumbano ya mitaani. Pamoja na hayo, hali hii inazidi kupunguza matumaini ya mchakato wa mageuzi ya utawala kutoka mikononi mwa Wanajeshi na kukabidhiwa raia.