Pakistan yakana ushirikiano na Taliban

Ripoti ya siri ya shirika la kujihami NATOkuhusu Afghanistan iliyopatikana na BBC inasema kua kundi la Taliban linapokea msaada wa moja kwa moja kutoka shirika la kijasusi la Pakistan la ISI,na kwamba linaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na raia wengi wa Afghanistan.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bi.Hina Rabbani na Rais Hamid Karzai

Wakati wa ziara yake isiyo ya kawaida nchini humo, Waziri wa mashauri ya nje wa Pakistan Bi.Hina Rabbani Khar alisema kua ripoti hio inafaa kupuuzwa akitoa mfano wa mvinyo wa kale kuwekwa ndani ya chupa ya kisasa.

Msemaji wa NATO mjini Kabul amesema kua ripoti hio sio tathmini ya matukio ya kijeshi bali ni maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wapiganaji wa Taliban waliozuiliwa.

Utafiti huo umefanywa baada ya kuwahoji wapiganaji wapatao elfu nne waliokamatwa pamoja na wanaharakati wanaolitumikia kundi la Al Qaeda.

Ripoti hio inabaini muundo na imani iliyopo kwa kundi la Taliban. Licha ya kipindi cha miaka kumi ya vita wapiganaji na viongozi wa kundi hilo hawajetetereka, wana uwezo wa kifedha na hawajakaribia kusalimu amri.

Halikadhalika wanaongozwa na kulindwa na Pakistan.

Waziri wa mashauri ya nje wa Pakistan, Hina Rabbanni Khar, akiwa ziarani mjini Kabul amesema madai hayo ni upuuzi".

Hata hivyo ripoti hii ndiyo ya kwanza iliyobaini na kutoa maelezo ya undani kuwahi kutolewa kuhusu hali halisi kuhusu kundi la Taliban. Haya ni matokeo ya kuwahoji watu 27,000. Ndani ya ripoti hii kuna viunga vya miji nchini Pakistan vilivyotajwa kua viongozi wa Taliban wamepewa hifadhi.

Nato linasema kua ripoti hio imetoa maelezo kuhusu Taliban na pia kutoa mwangaza wa jinsi raia wa Afghanistan wanavyozidi kuichukia serikali yao kwa kuiona kama iliyojaa ulaji rushwa, jambo linalowafanya raia walipendelee kundi la Taliban.

Hata wamo maofisa na askari wa vikosi vya serikali wanaoshirikiana na kundi hilo, ambalo wengi wana imani kua litarudi madarakani siku moja.