Mazishi ya jumla kwa waliouawa Nigeria

Mazishi Nigeria Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waombolezaji katika mazishi ya waliouawa Nigeria

Miili ya watu 18 waliouawa siku ya Krisimasi kwenye shambulio la bomu katika kanisa Katoliki mjini Abuja Nigeria imezikwa katika kanisa hilo.

Kundi la wapiganaji wenye siasa kali za kiislamu la Boko Haram limedai kuhusika na shambulio hilo lililouwa zaidi ya watu 40.

Kundi hilo linataka kulazimisha kuanzishwa kwa utawala unaozingatia sheria za Kiislamu nchini Nigeria.

Maelfu ya waombolezaji walihudhuria mazishi ya watu 18 waliouawa katika shambulio la bomu la siku ya Krismasi dhidi ya kanisa Katoliki la mtakatifu Theresa ,Madalla, karibu na mji mkuu Abuja.

Sehemu ya mbele ya kanisa hilo pia iliteketezwa katika mlipuko huo.

Baadhi ya waombolezaji walikusanyika nje ya kanisa hilo ambalo kawaida lina nafasi kwa waumini elfu tatu tu.

Misa ya wafu ilifuatiwa na kuzikwa kwa marehemu hao 18 katika kitalu cha kanisa hilo.

Miongoni mwa waombolezaji ni kijana mmoja ambaye ameiambia BBC kwamba amewapoteza dada zake 4 katika mlipuko huo na watano bado wanapatiwa matibabu hospitalini.

Ulinzi ulikuwa mkali katika eneo la kanisa hilo kama hatua ya tahadhari dhidi ya mashambulizi zaidi wakati wa mazishi hayo.

Watu wengi bado wana hasira dhidi ya jeshi la polisi la Nigeria kwa kuruhusu mtuhumiwa mkuu wa shambulio hilo la siku ya krismasi kutoroka kizuizi chao.

Kutoroka kwake kulisababisha mageuzi katika jeshi la polisi na kuteuliwa kwa mkuu mpya wa kikosi hicho.

Kikundi cha wanaharakati wa siasa kali za kiislamu Boko Haram kimehusika na mfululizo wa mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama na raia .

Mwishoni mwa wiki kililikataa ombi la Rais la kuzungumza katika juhudi za kukomesha mashambulizi hayo.