Madini ya chuma yaleta maafa Nigeria

Image caption Uchimbaji dhahabu Nigeria

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limesema kuwa shughuli ya uchimbaji dhahabu kaskazini mwa Nigeria imewasababishia maelfu ya watoto maradhi mabaya zaidi kutokana na uchafuzi wa madini ya chuma.

Human Rights Watch inasema kuwa uchafuzi huo ndio mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni na watoto wengi katika eneo hilo wanahitaji msaada wa kimatibabu.

Shirika hilo linasema tayari watoto mia nne wamekwishaaga dunia kutokana na mkasa huo.

Baadhi ya watoto hao ambao wana umri wa miaka minane wanafanya kazi katika migodi ya dhahabu katika jimbo la Zamfara.

Image caption Watato wanahusika katika uchimbaji dhahabu Nigeria

Viwango vya uchafuzi wa madini ya chuma ni vya juu zaidi katika baadhi ya vijiji na takriban asilimia arobaini ya watoto walioenekana kuwa na dalili ya kupata maradhi yanayotokana na uchafuzi huo wameaga dunia.

Shirika la Human Rights Watch linasema kuwa uchimbaji wa madini unawaweka watoto hao katika hatari ya kuathirika na vumbi ya madini hayo ya chuma ambayo inachafua maji pamoja na chakula..

Shirika la afya duniani WHO linasema kuwa madini ya chuma husababisha matatizo ya kudumaa ubongo na umbo la watoto.