Hague azuru Mogadishu

Image caption William Hague

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amefanya ziara nchini Somalia na kutoa wito wa kuimarishwa vita dhidi ya kundi la Alshabaab.

Bw. Hague amezuru Somalia huku mkutano maalumu kujadili mzozo wa nchi hiyo ukipangwa kufanyika baadaye mwezi huu.

Ulinzi ulikuwa mkali wakati waziri huyo alipowasili katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Hii ni kutokana na kuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu kutoka Uingereza kuzuru Mogadishu, katika kipindi cha miongo miwili.

Bwana Hague alisafiri katika msururu wa magari yenye ulinzi mkali kukutana na rais wa serikali dhaifu ya mpito ya Somalia, Sheikh Sharif Ahmed.

Waziri huyo wa Uingereza amesema nchi yake itafungua ubalozi mjini Mogadishu punde tu nchi hiyo itakuwa na usalama wa kuridhisha.

Mashambulizi ya kujitoa mhanga na makundi ya kigaidi yamefanya taifa hilo kuwa hatari zaidi duniani.

Ziara ya Bwana Hague inafanyika majuma machache kabla ya mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia utakaofanyika mjini London.

Lengo la mkutano huo wa February 23 ni kutatua mzozo wa kisiasa uliopo katika taifa hilo la pembe ya Afrika.

Maswala nyeti yatakayozungumziwa ni uharamia na jinsi ya kupambana na makundi ya kigaidi.