Vifo katika mji wa Suez nchini Misri

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Waandamanaji wakiwa juu ya ukuta unaozingira majengo ya wizara ya mambo ya ndani.

Watu wawili wameuwawa na wengine zaidi ya 400 wamejeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika kote nchini Misri baada ya vifo vya watu 74 waliuwawa baada ya mechi ya soka kati ya klabu mbili maarufu katika mji wa Port Said.

Watu hao wawili waliaga dunia baada ya kupigwa risasi na maafisa wa polisi waliokuwa wakijaribu kutawanya umati wa watu waliojawa na hasira katika mji wa Suez, maafisa wa afya wamesema.

Katika mji mkuu wa Cairo, maelfu ya waandamanaji wamesalia kwenye barabara za mji baada ya siku nzima ya makabiliano na maafisa wa polisi.

Maelfu walitembea kwa miguu hadi makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani, ambako maafisa wa usalama waliwafyatulia gesi ya kutoa machozi kuwatimua.

Awali, waziri mkuu wa Misri alitangaza kufutwa kazi kwa maafisa kadhaa wa ngazi ya juu.

Maziko ya baadhi ya waathiriwa hao 74 yalifanyika Port Said, ambako mechi hiyo ya 'mkosi' iliandaliwa siku ya jumatano.

Vifo hivyo vilitokea wakati mashabiki walivamia uwanja baada ya mchuano kati ya klabu maarufu kutoka Cairo al-Ahly na klabu ya Port Said al-Masry.

Risasi za moto

Wakati giza lilipoingia katika mji wa Cairo, maelfu kadhaa ya waandamanaji walisalia barabarani karibu na wizara ya mambo ya ndani, amesema mtu mmoja aliyeshuhudia purukushani hiyo.

Katika mji wa Suez, afisa wa afya Mohammed Lasheen alisema kuwa watu wawili waliuwawa kwa kupigwa risasi mapema Ijumaa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Makabiliano ya mjini Cairo

Mtu mmoja aliyeshuhudia kisa hicho amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema: "waandamanaji wanajaribu kuingia kwa nguvu katika kituo cha polisi cha Suez police na polisi sasa wanafyatua risasi za moto."

Siku ya Alhamisi, wafuasi wa klabu ya al-Ahly walikusanyika nje ya uwanja wa klabu hiyo mji Cairo mchana kutwa. Msururu wa maandamano ulifanyika hadi katika Medani ya Tahrir, na kisha hadi makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani.

Wengine waliimba nyimbo za kuwakashifu watawala wa kijeshi nchini Misri, wakati wengine wakirusha mawe.

"jeshi letu ni sharti lichagua kati ya baraza la kijeshi na wanamapinduzi,'' waliimba kwa sauti ya juu.

Polisi walifayatu hewa ya kutoa machozi kuwazuia waandamanaji hao kuingia katika majengo ya wizara, ambayo yamezingirwa na vizuizi vya ukuta.

Pikipiki ziliwasafirisha watu walijeruhiwa kutoka eneo la makabiliano huku magari ya ambulansi yakishindwa kufikia maeneo hayo.

Bado kuna watu waliokusanyika nje ya majengo ya wizara ya mambo ya ndani.

Mara kwa mara Ijumaa huwa ni siku hatari, na wakati swala ikitarajiwa kufanyika na kuwapa waandamanaji fursa ya kukusanyika tena, mjini Cairo na Suez makabiliano makali zaidi yanatarajiwa.