Homs yatwangwa kwa mizinga

Wanaharakati wanaopinga serikali ya Syria wanasema shambulio la jeshi dhidi ya mji wa Homs, limeuwa zaidi ya watu 200.

Haki miliki ya picha AFP

Wakaazi wa mji wanaeleza kuwa mtaa wa Khaldiyeh ulishambuliwa kwa mizinga mingi.

Ikiwa watu 200 watathibitishwa kuuwawa, basi itakuwa idadi kubwa kabisa kutokea katika siku moja tangu ghasia kuanza nchini Syria miezi 11 iliyopita.

Serikali ya Syria imekanusha kuwa iliipiga mabomu Homs.

Huku nyuma, Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema itakuwa aibu iwapo mswada wa azimio la Umoja wa Mataifa linalolaani utumizi wa nguvu wa serikali ya Syria, litapitishwa leo.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kujadili mswada huo, ambao unaunga mkono mpango wa Jumuia ya Nchi za Kiarabu, kumtaka rais wa Syria, Bashar al-Assad, akabidhi madaraka kwa naibu wake.

Bwana Lavrov alisema maneno yaliyotumiwa kwenye mswada huo, hayaridhishi nchi yake.

Urusi imesema azimio hilo lisitumike kuhalalisha jeshi la kigeni kuingilia kati Syria.

Urusi piya inapinga vikwazo vya silaha dhidi ya Syria, ambayo ni moja kati ya wateja wakubwa wa silaha za Urusi.