Utaliana yapata homa ya West Nile

Baridi ya juma hili Utaliana haikupata kuonekana kwa miaka 30.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Na huku Wataliana wanatetemeka, wamepata habari nyengine zisokuwa za kawaida: kwamba wageni wamewasili katika kisiwa cha Sardinia, kutoka Afrika.

Wingu la flamingo, au heroe, huvutia maelfu ya watu kila mwaka, watu wanaopenda kuwatazama kwenye kisiwa cha Sardinia, magharibi mwa Utaliana.

Lakini sasa, watafiti wanaonya kuwa flamingo na ndege wengine wanaohama-hama, wameleta mgeni mwengine asiyetakikana: yaani West Nile fever, au homa ya West Nile.

Homa hiyo inatapakazwa na virusi vinavobebwa na mbu, ambavyo mwanzo viligunduliwa Uganda.

Kinachowatia wasiwasi wakuu wa afya wa Sardinia, ni jinsi homa hiyo ilivotapakaa haraka ilipoathiri Uganda.

Vituo vya Marekani vinavyoshughulika na udhibiti wa magonjwa, vinasema watu wengi wanaoambukizwa homa ya West Nile hawapati athari yoyote mbaya - lakini kwa bahati mbaya wachache wanaoshikwa na homa, wanazirai na kutetemeka; wanapoteza macho kwa muda, hufa ganzi, na kupooza.

Tayari watu wane wamekufa tangu homa hiyo kuthibitishwa mwezi wa Septemba, kuwa imeingia Sardinia.

Kwa sasa baridi imezuwia homa hiyo kutapakaa zaidi, lakini kuna wasiwasi kuwa majira ya chipukizi yakianza, itachomoza tena.