Somalia kufukuza waliovamia majengo

Wakimbizi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi wa ndani wakipanga foleni ya chakula

Somalia imeanza shughuli kubwa ya kuwahamisha maelfu ya watu waliovamia na kuishi katika majengo ya serikali mjini Mogadishu.

Meya wa Mogadishu ameiambia BBC kuwa watakaohamishwa hawatapewa nyumba za kuhamia kwa sababu wavamizi hao wamekuwa wakilipa kodi kwa wamiliki "wasio halali".

Maelfu ya watu pia wanaishi kama wakimbizi katika jiji hilo baada ya kukimbia mapigano na ukame.

Hali ya usalama mjini Mogadishu imetengemaa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kundi la wanamgambo la al-Shabaab mwaka jana liliondoka mjini humo lakini bado linaendelea kufanya mashambulizi hasa ya kujitoa mhanga.

Wiki iliyopita, William Hague alikuwa waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Uingereza kuzuru Mogadishu tangu mwaka 1991 - mara ya mwisho Somalia kuwa na serikali inayofanya kazi.

Mashirika ya misaada ya nchini humo yanakadiria kuwa watu 50,000 wamekuwa wakijihifadhi katika majengo ya wizara mbalimbali, shule na vyuo vikuu - mengi ya majengo hayo yakiwa yameharibika vibaya kutokana na miaka mingi ya vita.

Shule moja iliwahi kutumiwa kama kambi ya muda na kuhifadhi takriban watu 17,000, wakimbizi wa ndani.

Meya wa Mogadishu Mohamud Nur ameiambia Idhaa ya Kisomali ya BBC kuwa watu wanahamishwa kutoka katika majengo ambayo serikali imepata fedha za kuyakarabati.

Fedha nyingi za shughuli hiyo zinatoka Uturuki.