Milipuko yarindima Nigeria

Nigeria Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kumekuwa na mfululizo wa mashambulio nchini Nigeria

Kituo cha polisi kimeshambuliwa na mlipuko na kusakamwa na watu wenye bunduki katika mji wa kaskazini wa Kano na kujeruhi afisa mmoja wa polisi.

Upande wa mashariki, katika muda huohuo, watu walioshuhudia wamesema wamesikia milipuko katika soko la mji wa Maiduguri.

Hisia za nani aliyeandaa mashambulio haya zitaelekea kwa kundi wa wanamgambo la Boko Haram.

Boko Haram imeanzisha uasi katika eneo hilo katika jitihada za kuin'goa serikali ya nchi na kuanzisha taifa la Kiislam.

Kano ilishuhudia mfululizo wa mashambulizi mwezi uliopita yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 185.

Shambulio katika kituo cha polisi limetokea katika wilaya ya Sharada iliyopo Kano jioni ya saa kumi na mbili saa za huko.

Watu wenye silaha wakiwa na mabomu pia walikivamia kituo hicho kutoka pande mbalimbali, kwa mujibu wa msemaji wa polisi Magaji Musa Maji'a, akizungumza na shirika la habari la Reuters.

"Polisi mmoja alipigwa risasi mguuni na anapatiwa matibabu hospitalini," alisema.

Mkazi mmoja aitwaye Bala Salisu aliliambia shirika la habari la AFP kuwa alikuwa ndio kwanza ameingia nyumbani kwake kutekeleza amri ya kutotembea usiku aliposikia mlipuko mkubwa.

"Muda mfupi baadaye milio ya risasi ilisikika. Jinsi nilivyosikia ilikuwa kama wanajibizana kwa risasi," alisema.

Mwandishi wa habari wa Reuters katika eneo hilo amesema mlipuko ulikuwa na nguvu kiasi cha kutikisa madirisha, na kufuatiwa na mapambano ya risasi yaliyodumu kwa zaidi ya saa moja.

Magaji Musa Maji'a amesema maafisa wa polisi hatimaye walidhibiti hali ya kituo hicho.

Wakati huohuo katika mji wa Maiduguri - ambao ndio ngome ya Boko Haram - mfululizo wa milipuko imesikika katika eneo la sokoni na moshi mweusi ulionekana ukitanda katika eneo hilo.