Capello ajiuzulu kuifundisha England

Capello aamua kuachia ngazi Haki miliki ya picha PA
Image caption Capello aamua kuachia ngazi

Fabio Capello amejizulu ukocha wa England, Chama cha soka cha England FA, kimethibitisha.

Capello amejiuzulu baada ya kukutana na mwenyekiti wa FA David Bernstein na katibu mkuu Alex Horne, kwenye makao makuu ya chama hicho yaliyopo kwenye uwanja wa Wembley, London.

Taarifa ya FA imesema: "Chama cha soka kinathibitisha kuwa Fabio Capello amejiuzulu leo umeneja wa England."

Siku ya Jumatatu, Muitaliano huyo aliupinga waziwazi uamuzi wa FA wa kumvua John Terry unahodha.

Taarifa ya FA imeendelea kusema: "Majadiliano yalilenga kuhusu uamuzi wa bodi ya FA wa kumvua unahodha John Terry, na pia majibu ya Fabio Capello kupitia televisheni ya Italia.

"Katika mazungumzo yaliyodumu zaidi ya saa moja, kujiuzulu kwa Fabio kulikubaliwa na ataachia nafasi hiyo mara moja."

Bernstein alisema: "Ningependa kusisitiza kuwa wakati wa mkutano na wakati wote akiwa meneja wa England, Fabio amekuwa akiwajibika kitaalam.

"Tumekubali hatua ya kujiuzulu kwa Capello, tukikubaliana kuwa ni uamuzi sahihi. Tungependa kumshukuru Fabio kwa kazi yake kwa timu ya England na kumtakia kila la heri katika siku zijazo."

Mkutano wa Bernstein, utawala wa timu ya England na waandishi wa habari utafanyika Wembley siku ya Alhamisi.

FA haitasema lolote zaidi hadi katika mkutano huo.

Mkutano wa FA na Capello ulikuwa wa kwanza tangu FA ilipomvua unahodha Terry ambaye anasubiri matokeo ya kesi yake mahakamani itakayosikilizwa mwezi Julai.

Terry, 31, anakana mashtaka ya kumtolea maneno ya kibaguzi mchezaji wa QPR, Anton Ferdinand.

Siku ya Jumapili, meneja wa England, Fabio Capello alikiambia kituo cha TV cha taifa cha Italia, RAI, kuwa haamini mtu anapaswa kuadhibiwa na mamlaka za michezo kabla ya mahakama kutoa hukumu.