Ujumbe wa Kiarabu kwenda tena Syria

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon Haki miliki ya picha Getty
Image caption Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema jumuiya ya nchi za kiarabu ina mipango ya kurejesha tena wawakilishi nchini Syria na kuwa jumuiya hiyo imeitisha usaidizi wa umoja wa mataifa.

Katibu huyo alisema kwamba mkuu wa jumuiya hiyo Nabil el-Arabi alikuwa amemwambia kuwa alitaka kutuma tena ujumbe wa jumuiya ya nchi za Kiarabu nchini Syria lakini ulikwama kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Bwana Ban amesema uamuzi wa serikali za Urusi na Uchina kutumia kura zao za turufu kupinga vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Syria, umeifanya serikali ya nchi hiyo kuimarisha dhuluma dhidi ya raia wake.

Serikali za magharibi kwa sasa zinafatuta njia ya kumaliza mgogoro huo.

Majeshi ya serikali ya Syria yameendelea kushambulia maeneo yanayomilikiwa na vikundi vya upinzani.

Wanaharakati wanasema wanajeshi waliendelea kuushambulia mji wa Homs kwa makombora siku ya Alhamisi.

Maeneo kadhaa mjini Homs yanadhibitiwa na vikundi vya waasi , ikiwa ni pamoja na majeshi ya serikali yaliyoasi. Jambo hili limefanya mji huo kuwa kitovu cha wanaompinga Rais Bashar al-Assad.

Zaidi ya watu 50 waliuawa mjini Homs siku ya Jumatano pekee, kwa mujibu wa shirika moja la haki za kibinadamu lenye makao makuu nchini Uingereza.

Akizungumza katika ofisi za Umoja wa Mataifa, Bwana Ban alisema: "Mateso ambayo raia wa Syria mjini wa Homs wamekumbana nayo ni ishara ya mambo mabaya zaidi ambayo huenda yakatokea siku zijazo."