Kanisa Katoliki kutoa mafunzo

Kanisa Katoliki limezindua mradi mpya wa kutoa mafunzo kwenye mtandao wa Internet unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani ambao unalenga kuwafunza maaskofu wa kanisa hilo jinsi ya kukabiliana na makasisi wanaowadhulumi watoto kimapenzi.

Tayari dhuluma za kingono zimeligharimu kanisa Katoliki zaidi ya dola bilioni mbili kote duniani kupitia malipo ya fidia kwa waathiriwa wa uovu huo.

Tangazo hilo limetolewa baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku nne huko Vatican kuhusu jinsi ya kuwalinda waathiriwa.

Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa kanisa katoliki na maaskofu kutoka zaidi ya mataifa mia moja.

Kwa mara ya kwanza, mwathiriwa mmoja aliyedhulumiwa kingono Marie Collins kutoka Ireland, alikuwa na wakati wa kueleza yaliyomsibu.

Collins alikuwa na miaka 13 wakati kitendo hicho kilipotokea, ''nadhani kuna watu walioko kwenye kanisa ambao sasa wanafahamu kwamba tatizo hili lipo...kuna haja ya kuwajibikia yaliyotendeka siku za nyuma.''

Kiongozi wa mashtaka wa Vatican, Charles Scicluna aliambia kongamano hilo kwamba amepokea ripoti zaidi ya elfu nne kwa kipindi cha miaka kumi imepita.

Inatarajiwa kwamba papa mtakatifu atapewa ripoti kamili kuhusiana na mkutano huo.