Kimbunga chaathiri Madagascar

Kimbunga Giovanna Haki miliki ya picha
Image caption Kimbunga Giovanna

Kimbunga chenye upepo mkali wa mwendo wa kilomita 194 kwa saa kimeathiri kisiwa cha Madagascar kwa kung'oa miti na vifaa vya kusafirisha umeme.

Kimbunga hicho, ambacho kimepewa jina Giovanna kilianza kwa kuathiri mji wa Toamasina, mashariki mwa kisiwa hicho.

Magari ya huduma za dharura yameonekana jijini Antananarivo yakiondoa vifusi.

Wataalam wa masuala ya hali ya hewa wanaonya kwamba uharibifu katika kisiwa hicho huenda ukawa mbaya kama ule wa 1994 , wakati kimbunga kilipowaua watu 200 na kuwaacha wengine 40,000 bila makaazi.

Afisa mmoja wa serikali ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Takriban mtu mmoja amefariki dunia katika mji wa Brickaville baada ya kuangukiwa na nguzo ya umeme.

Watu wamebakia majumbani mwao kwa sababu ofisi, shule na biashara zimefungwa na umeme umekatika.