Demokrasia sio muhimu kwa sasa Libya

Wananchi wengi wa Libya wanapendelea uongozi thabiti badala ya demokrasia licha ya kutawaliwa kwa miaka 40 na Muammar Gaddafi, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kote nchini humo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wengi hawaelewi demokrasia

Ni asilimia 15 tu kati ya watu elfu mbili waliohojiwa na wanavyuoni kutoka Benghazi Libya na Oxford Uingereza walisema kwamba wangependelea mfumo wa kidemokrasi ukianzishwa mwaka ujao.

Zaidi ya asilimia 40 waliunga mkono uongozi thabiti wa mtu ama kikundi kimoja.

Hata hivyo takriban theluthi nzima ya waliohojiwa walisema wangependelea serikali ya kidemokrasia katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Licha ya kwamba wengi wamesema wangependa kuona uongozi thabiti ukishika hatamu, asilimia 69 pia wamesema wanaamini raia wa kawaida wanapaswa kuchangia mawazo yao kuuhusu jinsi Libya inavyoendelea.

Na asilimia 16 ya wanananchi wamesema wako tayari kutumia nguvu ili kupigania malengo yao ya kisiasa.

Watafiti wanasema hii inamaanisha kuwa takriban watu 630,000 walio tayari kubeba silaha mbali na wale 280,000 walioasi dhidi ya utawala wa Gaddafi.

Dk Christoph Sahm wa chuo kikuu cha Oxford amesema utafiti huo umaonyesha kua wananchi wa Libya hawaelewi jinsi demokrasia inavyofanya kazi.

Dr Sahm ameongeza kuwa utafitif huo unabainisha hatari iliyopo dhidi ya utulivu wa baadae kwa kuwa idadi kubwa ya watu wanasema wako tayari kubeba silaha kutetea haki zao.

Hata hivyo takriban asilimia 80 ya waliohojiwa walisema shauku yao katika siasa imeongezeka tangu mapinduzi yaliyoanza mwaka mmoja uliopita katika mji wa Mashariki wa Benghazi na yaliyomalizika pale Gaddafi alipouwawa mnamo mwezi wa October.