Mnigeria wa al-Qaeada afungwa maisha

Abdulmutallab Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Abdulmutallab ni mtoto wa mfanyakazi wa benki wa Nigeria

Raia mmoja wa Nigeria anayetuhumiwa kujaribu kulipua ndege inayokwenda Marekani siku ya Krismasi mwaka 2009, amehukumiwa kifungo cha kwenda jela maisha.

Umar Farouk Abdulmutallab, 25, alikiri kosa la kujaribu kulipua ndege ya abiria akiwa kama mfuasi wa kundi na kutekeleza njama za al-Qaeda.

Familia yake mara moja imetaka serikali ya Marekani kupitia upya hukumu hiyo.

Abdulmutallab aliungua wakati bomu lililokuwa limeshonwa ndani ya nguo yake ya dani kushindwa kulipuka kikamilifu, wamesema waendesha mashtaka.

Watu wapatao 300 walikuwemo ndani ya ndege hiyo ikitokea Amsterdam kwenda Detroit.

Baadhi ya abiriwa walikuwepo mahakamani hapo wakati jaji Nancy Edmunds akitoa hukumu hiyo.

"Hili lilikuwa tukio la kigaidi ambalo hatuwezi kulikwepa tu," alisema Jaji Edmunds, wakati akisoma hukumu hiyo ya juu kabisa.

Akiwa mtoto wa mfanyakazi wa benki nchini Nigeria, na mwanafunzi katika chuo kikuu cha London, Abdulmutallab alikabiliwa na mashtaka manane, yakiwemo ya ya ugaidi na kutaka kuua.

Kundi la al-Qaeda tawi la rasi ya Uarabuni, lenye makao yake nchini Yemen lilisema lilihusika na jaribio hilo.

Katika taarifa yake kwa BBC, familia ya Abdulmutallab imesema "wanamshukuru Mungu kwa sababu tukio hilo baya halikusababisha majeraha au kifo".