Al-Shabaab watimuliwa Baidoa

Majeshi ya Ethiopia na yale ya serikali ya mpito ya Somalia yameuteka mji wa Baidoa ambao ni mojawapo ya ngome kuu ya wapiganaji wa Al Shabaab.

Walioshuhudia wamesema takriban magari 50 vikiwemo vifaru vya kivita viliingia mjini Baidoa bila upinzani wowote.

Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu amesema Baidoa ni ngome muhimu ya wapiganaji hao eneo lingine likiwa bandari ya Kismayo kusini mwa nchi.

Kundi la Al-Shabaab ambalo lilijiunga rasmi ya mtandao wa al-Qaeda limethibitisha kuwaondoa wapiganaji wake kutoka mji huo. Wapiganaji hao aidha wameonya kuanzisha mashambulio ya kujitoa mhanga dhidi ya majeshi ya kigeni.

Kutekwa kwa mji wa Baidoa ni pigo kubwa kwa Al Shabaab kwani ni makao ya mmoja wa viongozi wa kundi hilo Abu Mansoor na baadhi ya wanachama wengine wa juu.

Awali Al Shabaab ilionya umwagikaji mkubwa wa damu ikiwa mji huo utalengwa na majeshi ya serikali.

Matukio haya yamejiri mkesha wa kongamano la kimataifa kujadili mstakhabali wa Somalia mjini London, Uingereza ambapo zaidi ya viongozi 40 wa dunia wanatarajiwa kuhudhuria.