Mkutano London: 'Wasomali tumieni fursa'

Haki miliki ya picha PA
Image caption Viongozi wa dunia wataka Somalia kutumia fursa hii kujenga Taifa lao

Viongozi wa dunia wamewataka Wasomali kutumia ‘fursa hii adhimu’ kulijenga upya taifa lao, wakati wa mkutano maalum mjini London kujadili mustakabali wa Taifa hilo lililoharibiwa na vita.

Kumaliza vitisho vya ugaidi na uharamia ni kwa maslahi ya kila mmoja, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alisema.

Hillary Clinton, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani alisema mipango ya kuchagua viongozi na kupata katiba mpya kabla ya mwezi Agosti ni ‘kunia makuu’.

Lakini Bi Clinton alisema jukumu la serikali ya mpito inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa haitaongezewa muda wake.

Somalia imekuwa katika miongo zaidi ya miwili ya vita na njaa.

Wawakilishi kutoka makundi mengi ya Wasomali walihudhuria mkutano huo lakini kundi la wapiganaji wa kiislam wa al-Shabab linalodhibiti sehemu kubwa ya kati na kusini mwa nchi halikualikwa.

Uingereza imeielezea Somalia kama ‘taifa lililoshindwa vibaya duniani’ lakini ikasema linahitaji ‘fursa nyingine.’

Bw Cameron aliwaambia viongozi waliohudhuria mkutano huo, ambao Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, kiongozi wa Ethiopia Meles Zenawi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakiwa miongoni mwa waliohudhuria, kuwa dunia italipa gharama kubwa iwapo itapuuzia hatma ya Somalia.

"Katika nchi ambayo kuna matumaini madogo, ambapo kuna ghasia vurugu na ugaidi, na uharamia unaoharibu njia muhimu za kibiashara kuwateka watalii’ alisema.

"Mawazo ya vijana yanaharibiwa na siasa kali, kuzaa ugaidi ambao unatishia sio tu Somalia lakini kwa ulimwengu mzima. Iwapo sisi wote tutakaa tu na kuangalia, tutalipa gharama kwa kuyaacha yaendelee."

Wakati wa hotuba yake, Rais waSomaliaSheikh Sharif Sheikh Ahmed alitoa wito wa kumalizika kwa marufuku ya silaha, akisema: "Tunatafuta usalama. Tunahofu na kitakachotokea."

Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha maamuzi ya kuongeza idadi ya askari wa kulinda amani katika vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia wapatao 5,000 kwa wale zaidi ya 17,000 walioko huko.

Wajumbe wa Baraza hilo wamekubaliana kutoa fedha zaidi kwa ujumbe huo na kuongeza muda wa majukumu yake huko.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Somalia na Waziri Mkuu katika mkutano wa London

Yoweri Museveni, kiongozi wa Uganda– ambaye ametoa wanajeshi wengi kwenye vikosi vya Umoja wa Afrika nchiniSomalia– ameuambia mkutano huo kuwa suluhu ya matatizo ya Afrika inaweza kupatikana vizuri kutoka kwa waafrika wenyewe.

'Hakuna mazungumzo na wapiganaji'

Wakati huo huo vikosi vya Ethiopia na Somalia vimeuteka mji ngome ya al-Shabab wa Baidoa kusini magharibi mwa nchi ambao karibuni walijitokeza kuwaunga mkono al-Qaeda.

Jumatano jioni maafisa walisema bomu lililotegwa na wanamgambo hao lilipuka katikati ya mji wa Baidoa na kusababisha majeraha kidogo.

Wapiganaji hao ambao wamekuwa wakipambana na serikali ya mpito tangu mwaka 2007 wamesema mkutano wa London ni majaribio mengine ya kuitawala Somalia.

"Wanataka sisi tuwe chini yao na hatutaruhusu hilo. Mungu akipenda tutakabiliana na matokeo yake kwa nguvu zote kuzima," alisema msemaji wa al-Shabab Ali Mohamud Rage.

"Marekani yenye nguvu ilishindwa na hawa waafrika wote wameshindwa na tunasema msipoteze muda wenu, mtashindwa. Tena tunawaambia wasipoteze raslimali zao."

Katika hotuba yake, Bibi Clinton alisema Marekani hatafanya mazungumzo na al-Shabab, lakini alisema ni wakati muhimu kwa Somalia kufanya maendeleo.

"Kwa miongo mingi, dunia imelenga katika kile tunachoweza kukizuia kutokea nchiniSomalia–iwe migogoro, njaa, na majanga mengine," Shirika la habari la AFP limemnukuu akisema.

"Sasa tunalenga katika kile tunachoweza kukijenga. Fursa hii ni halisi"

Viongozi wa Somalia wamesema changamoto zake haziwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi pekee na malengo hayana budi kuwa kwenye misaada ya kibinadamu, elimu na sheria na utulivu.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Somalia na eneo linalodhibitiwa na Al-Shabab

Licha ya kuondolewa kwa nguvu kutoka mji mkuu Mogadishu, mwaka jana, al-Shabab wameendelea kufanya mashambulzi katika mji huo.