Maafisa wa NATO wauwawa Afghanistan

Majeshi ya kigeni yanayongozwa na NATO nchini Afghanistan, yanasema wanajeshi wake wawili waliuwawa kwa kupigwa risasi ndani ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi, mjini Kabul.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Taarifa yao ilisema kuwa mtu mmoja aliwapiga risasi maafisa hao wawili; lakini haikuelezwa ni nani.

Maandamano ya fujo yamendelea kwa siku ya tano nchini Afghanistan, kulalamika juu ya kuchomwa Koran kwenye kambi ya jeshi la Marekani.

Taarifa zinaeleza kuwa watu kama 6 wameuwawa, na wengine kadha kujeruhiwa, katika mapambano baina ya polisi na waandamanaji.

Maelfu ya watu walikusanyika karibu na uwanja wa jengo la Umoja wa Mataifa, katika mji wa Kunduz, kaskazini mwa nchi.

Watu waliokuwa na hasira waliirushia mawe nyumba ya gavana wa jimbo la kati, la Laghman.

Watu kama 23 wamekufa hadi sasa, pamoja na wanajeshi wawili wa Marekani.