Waasi Sudan washambulia majeshi ya serikali

Muungano wa makundi ya waasi nchini Sudan umesema kuwa umeanzisha operesheni ya pamoja ya kijeshi.

Muungano wa makundi ya waasi Sudan Revolutionary Front, ambao unajumuisha makundi ya waasi kutoka maeneo tofauti ya nchi umesema umeshinda makabiliano kati ya wapiganaji wake na vikosi vya serikali.

Wasemaji kutoka makundi hayo walisema kundi la waasi la JEM kutoka Darfur pamoja na kundi la SPLM- North yalishambulia vikosi vya serikali katika eneo la Kordofan Kusini.

Makundi hayo yanasema yalishinda makabiliano hayo kwenye ziwa la Abriad.

Hii ndio mara ya kwanza makundi ya waasi yameshirikiana katika vita tangu kuundwa kwa muungano wa makundi ya waasi, Sudan Revolutionary Front, mwaka uliopita.

Msemaji wa jeshi ya Sudan alikiri kuwa vikosi vyake vilishambuliwa na JEM na SPLM-North. Alishutumu Sudan Kusini kwa kushiriki kwa shambulizi hilo.

Sudan huwa inaishutumu Sudan Kusini kwa kuunga mkono mshiriki wake wa zamani SPLM-North, katika eneo la Kusini mwa Kordofan na pia kwenye eneo la Blue Nile.

Hata hivyo hatukuweza kupata fursa ya kuzungumza na msemaji wa jeshi la Sudan Kusini lakini serikali imekuwa ikipinga madai hayo ya kuunga mkono waasi.

Shambulizi hilo lililotekelezwa na muungano wa makundi ya waasi litazua wasiwasi hasa mjini Khartoum lakini makundi hayo yako mbali na kuafikia ndoto yao ya kumngoa madarakani rais Omar el Bashir.