Mkuu wa kituo cha Rediyo auawa Somalia

Uhuru wa wandishi habari Haki miliki ya picha BBC World Service Trust
Image caption Uhuru wa wandishi habari matatani

Mkuu wa kituo cha Rediyo moja nchini Somalia iliyofungwa na kundi la Al Shabaab ameuawa nje ya nyumba yake, mtu aliyeshuhudia tukio hilo ameiambia BBC.

Mtu huyo amesema kua Abukar Hassan Kadaf alipigwa risasi na watu wawili waliokua na bastola katikati ya mji mkuu Mogadishu.

Bw.Kadaf aliiongoza Rediyo ya Somaliweyn hadi ilipoporwa na kundi la al-Shabab mnamo mwaka 2010 kundi hilo lilipodhibiti mji huo.

Baadaye alishiriki siasa za mitaa lakini marafiki zake wamesema kua alikua na mipango ya kufufua kituo chake cha Rediyo.

Somalia ni nchi isiyo na serikali ya uhakika kwa zaidi ya miaka 20 sasa na ni mojapo ya nchi hatari kwa wandishi habari kufanya kazi.

'Msiba'

Mwezi uliopita mkuu wa mtandao wa vyombo vya habari, Hassan Osman Abdi, aliutejulikana pia kama "Hassan Fantastic", aliuawa kwa risasi nje ya nyumba yake na watu watano waliokua na silaha.

Aliyeshuhudia tukio la hivi karibuni ameiambia idhaa ya Kisomalia ya BBC kua watu hao walimpiga risasi kadhaa Bw.Kadaf ikiwa saa kumi na mbili za huko Somalia.

"mauwaji haya ... Ni msiba mwingine unaozidi kuangamiza uhuru wa vyombo vya habari nchini Somalia," Alisema Omar Faruk Osman, katibu mkuu wa shirika la wandishi wa habari la Somalia(NUSOJ)

Mauwaji ya kisiasa yamekua yakifanyika nchini Somalia katika kipindi cha miongo miwili ya makundi mengi yanayozozana.

Kundi la Al-Shabab, ambalo hivi karibuni lilijiunga na mtandao wa al-Qaeda mapema mwezi huu, lilijiondoa kutoka makao yake mjini Mogadishu mnamo mwezi Agosti mwaka jana katika kile kilichotajwa na kundi hilo kama kuondoka kwa ujanja na tangu hapo limekua likifanya mashambulio ya mara kwa mara katika mji huo.