Mitt Romney ashinda uteuzi wa Republican

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mitt Romney ashinda uteuzi wa chama cha Republican jimbo la Michigan

Mgombea anayepigiwa upatu kushinda uteuzi wa urais wa chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa mwezi novemba nchini Marekani, ameshinda uteuzi wa chama hicho katika jimbo la Michigan alikozaliwa.

Romney alishinda uteuzi huo baada ya kinyanganyiro kikali dhidi ya mpinzani wake wa karibu Rick Santorum.

Ushindi huo katika jimbo la Michigan umeonekana kuwa muhimu kwa bwana Romney kujikatia tikiti ya chama hicho kupambana na rais Barrack Obama.

Ameshukuru waliompigia kura na kuahidi kuendelea na juhudi zake za kutafuta uungwaji mkono.

Wachanganuzi wa masuala ya kisaisa wanasema ushindi wa Romney utampa nguvu zaidi hasa kwa kuwa kura za maoni zilikuwa zimeashiria kuwa mgombea mwenzake Bw Santorum huenda angeshinda.

Mitt Romney vile vile ameshinda uteuzi wa chama hicho katika jimbo la Arizona.