Shirika la ICRC laruhusiwa kuingia Homs

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Gari la kubebea wagonjwa mahututi

Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema kuwa limeruhusiriwa kuingia katika eneo la Baba Amr wilaya ya Homs, inayokabiliwa na mapigano makali.

Shirika hilo linatarajiwa kusafirisha misaada ya vyakula na dawa na pia kuwahamishwa waliojeruhiwa kutoka maeneo hayo.

Tangazo hilo limetolewa siku moja tu baada wa wapiganaji wa waasi nchini humo kutangaza kuwa wanajiondoa kutoka eneo hilo.

Wanaharakakti wa kijamii nchini humo wanasema wanajeshi wa serikali wameingia katika eneo hilo kwa fujo na kuwadhulumu.

Wakati huo huo, waandishi wawili wa habari kutoka ufaransa Edith Bouvier na William Daniels waliokuwa wamekwama mjini Homs kwa muda wa wiki moja sasa wametorokea nchi Jirani ya Lebanon.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amesema kuwa Edith Bouvier ambaye ni mwandishi aliyepata majeraha, anatarajiwa kuhamishwa hadi ufaransa kwa matibabu zaidi.

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limeitaka serikali ya Syria kuruhusu mashirika ya kutoa misaada nchini humo mara moja.

Wito huo umeungwa mkono na washiriki wakuu wa syria katika baraza hilo la Usalama, China na Urusi ambao wamepinga vikwazo na mikakati ya kijeshi nchini Syria.