Haki zakiukwa na wote Libya

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kibinaadamu nchini Libya, imeamua kuwa haki zilikiukwa pande zote mbili wakati wa vita vya kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.

Haki miliki ya picha

Ripoti hiyo ilichapishwa na Shirika la Haki za Kibinaadamu la Umoja wa Mataifa, lenye makao makuu mjini Geneva.

Ripoti hiyo piya inailaumu NATO, kwa kutochunguza mashambulio yake ya ndege, ambapo raia piya waliuwawa.

Ripoti hiyo inawalaumu wanajeshi wa Kanali Gaddafi kwa kuwauwa watu wengi, kuwabaka wengine ambao wametoweka, mateso na kunajisi watu - na kwamba vitendo hivyo vilifanywa kwa mpango katika mashambulio dhidi ya raia.

Wapiganaji wa zamani, ambao wakiitwa "thuwar", piya walifanya uovu vitani; pamoja na mauaji kinyume cha sheria, kuwakamata watu kiholela, mateso, mashambulio na wizi wa ngawira.

Baadhi ya vitendo hivo vinaendelea hadi leo, ripoti inasema.

Kuhusu kifo cha Kanali Gaddafi mwenyewe, wachunguzi wanasema hawakuruhusiwa kuona ripoti ya daktari aliyekagua maiti, ingawa wamewaomba wakuu mara kadha.

Picha zilizopigwa wakati alipokamatwa na kuuwawa, zilionesha kiongozi huyo wa zamani wa Libya, akibumundwa na kundi la wapiganaji wenye hasira.

Ripoti hiyo piya inasema ingawa ndege za NATO zililenga mashambulio vema, lakini wakati mwengine raia waliuwawa - 60 kwa jumla na 55 walijeruhiwa.