Wanajeshi watangaza mapinduzi Mali

Wanajeshi waasi wametangaza katika televisheni ya taifa ya Mali kuwa wamechukua udhibiti wa nchi, saa kadha baada ya kuvamia kasri ya rais.

Wanajeshi walioasi wanasema kuna marufuku ya kutotoka nje katika nchi nzima na kwamba katiba haitatumika kwa sasa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Marufuku kutoka nje nchini Mali

Siku ya Jumatano wanajeshi hao walifyatuliana risasi na wanajeshi watiifu kwa serikali.

Wanasema serikali haijawapa silaha za kutosha kukabiliana na waasi wa jamii ya Tuareg.

Tayari walikuwa wamechukua udhibiti wa kituo cha taifa cha redio na televisheni na kusitisha matangazo.

Baada ya saa kadha ya kuonyesha picha za nyimbo za wanamuziki wa Mali, kundi la wanajeshi likaonekana kwenye televisheni mapema siku ya Alhamisi, wakitambulishwa kama "Kamati itakayorudisha Demokrasia na kutuliza hali katika nchi".

Msemaji wa waasi hao, aliyetajwa kwa jina la Luteni Amadou Konare, alisema sasa wamemaliza "utawala usio thabiti" wa Rais Amadou Toumani Toure.