Sudan na Sudan kusini zapigana vikali

Haki miliki ya picha spl arrangement
Image caption wapiganaji wakikabila wa Sudan Kusini

Mapigano mapya yamizuka kati ya majeshi ya Sudan na yale ya Sudan kusini .

Pande zote zinasema kuwa mapigano hayo yametokea katika maeneo kadhaa ya mipaka kati ya mataifa hayo mawili.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema mapigano hayo ndio makubwa na mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu nchi hiyo ijipatie uhuru wake toka Sudan.

Na kuchipuka kwa mapiganao hayo mapya kumemfanya Rais Salva Kiir kuonya kuwa vita vinanukia eneo hilo

Rais Kiir amesema," asubuhi hii anga yetu ilishambuliwa kwa mabomu ....Ni katika maeneo ya Unity.

"Kiongozi huyo wa Sudan kusini amesema ni vita ambavyo wanalazimishwa kuwa navyo. Na ni Sudan ndio inatafuta vita hivyo"

Nae msemaji wa jeshi la Sudan amenukuliwa akisema kuwa vita viko katika maeneo ya South Kordofan na kusini mwa jimbo la Unity.

July mwaka jana Sudan kusini ilijitenga rasmi na Sudan baada ya vita vya miaka mingi.

Licha ya kujitenga huko kumekuwa na malumbano ya kisiasa na mikwaruzano kati ya nchi hizo mbili kutokana na sababu kadhaa lakini kubwa zaidi ikiwa ni zogo la mafuta.

Radio ya kitaifa ya Sudan imetangaza kuwa Rais Omar el-Bashir amehairisha ziara yake ya kwenda Sudan Kusini.

Vita hivi pia vinakuja wakati mkutano ulikuwa umepangwa kufanyika wiki ijayo kati ya Bashir na mwenzake wa Sudan Kusini ,Salva Kiir ili kusuluhisha sintofahamu kati ya nchi hizo mbili jirani