Maharamia wateka meli pwani ya Maldives

maharamia waimarisha harakati zao Haki miliki ya picha crown

Maharamia wa Kisomali wameiteka nyara meli ya mizigo unayomilikiwa na Iran katika pwani ya kisiwa cha Maldives. Kwa mujibu wa idara ya ulinzi ya Maldives, hii ndio mara ya kwanza maharamia hao kutoka Somalia wameteka nyara meli ndani ya maji yake.

Chombo hicho kwa jina MV Eglantine, kilitekwa nyara katika kisiwa cha Hoarafush, kaskazini magharibi mwa Maldives. Katika miaka ya karibuni maharamia wa Kisomali wameimarisha harakati zao katika Bahari Hindi.

Maafisa wa Maldives wametuma manowari yake katika eneo la tukio ambapo inashirikiana na India kujaribu kuwaokoa mabaharia waliomo ndani ya meli hiyo.Mnamo mwezi Novemba serikali ya Maldives ilitangaza kuanzisha mikakati ya kukabiliana na maharamia wa Kisomali ambapo inashirikiana na India pamoja na Sri Lanka.

Kisiwa cha Maldives kinapatikana kilomita 3000 kutoka pwani ya Somalia. Maharamia wameanza kutumia mashua kubwa na vifaa vya kisasa vinavyonunuliwa na kikombozi kinachotolewa kuwaachia mateka.