Muungano wa Afrika umeeleza wasiwasi wake juu ya mapigano kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Image caption Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping

Muungano wa Afrika umeeleza wasiwasi wake juu ya mapigano kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Kufuatia siku mbili za makabiliano, mkuu wa Muungano wa Afrika Jean Ping ameomba nchi zote mbili kuheshimu makubaliano ya kuondoa vikosi vyao hadi umbali wa kilomita 10 kutoka mpakani.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa mapigano yamesitishwa chini, lakini Sudan ilifanya mashambulio ya angani katika maeneo ya Sudan Kusini usiku.

Nchi hizo mbili zilipigana vita ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe kabla ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan.

Mapigano hayo, yaliyoanza siku ya Jumatatu, yanalenga maeneo yenye visima vikuu vya mafuta vya Heglig na jimbo la Unity, Sudan Kusini.

Gideon Gatpan, waziri wa mawasiliano wa jimbo la Unity, alisema siku ya Jumatano kuwa ndege za Sudan zilishambulia eneo lililoko kilomita 35 kutoka mji mkuu wa jimbo hilo la Unity, Bentiu, usiku, lakini vita ya chini imesitishwa.

Kutokana na hilo Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameahirisha ziara yake ya kwenda Sudan Kusini wiki ijayo, ambapo alitarajiwa kuhudhuria mkutano pamoja na mwenzake, Salva Kiir.

Lakini maafisa wa serikali wa nchi hizo mbili wanatarajiwa kukutana katika mji mkuu wa Ethiopia,Addis Ababa baadaye wiki hii kwa mazungumzo yenye nia ya kutuliza uhasama uliopo kwa sasa.