Majaji wa kesi ya Uhuru na Ruto tayari

Baada ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kumpata na hatia mwanasiasa maarufu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Thomas Lubanda, sasa mahakama hiyo inaelekea kukaza kamba kwenye shingo za vigogo wanne wa Kenya.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta akiwa ICC

Sasa ICC imetangaza jopo la majaji watatu watakaoanza kusikiliza kesi ya uhalifu wa kimataifa inayowakabili Naibu waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na mbunge William Ruto.

Wegine wanaokabiliwa na mashitaka kama hayo ni aliyekuwa Mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura, na mwanahabari Joshua arap Sang.

Mapema mwaka huu mahakama ya ICC iliamua kuwa Uhuru Kenyatta na wenzake watatu wanastahili kufunguliwa mashitaka kuhusiana na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya.

Katika machafuko hayo zaidi ya watu 1,130 waliuwawa huku wengine zaidi ya laki sita wakufurushwa makwao na mali za mamilioni ya pesa kuharibiwa.

Kuteuliwa kwa majaji hao wanne kunamaanisha kuwa kesi dhidi ya Naibu Waziri wa Kenya Uhuru Kenyatta na wenzake inasubiri tu kupangiwa tarehere ya kusikilizwa.

Majaji waliopangiwa kusikiliza kesi hizo ni Bi Christine Van den Wyngaert kutoka Ubelgiji,Bi Kuniko Ozaki kutoka Japani na bwana Chile Eboe-Osuji kutoka Nigeria.

Hatua hii inakuja wakati wanasiasa na viongozi kutoka eneo la kati la Kenya wakitangaza kampeni ya kutaka kesi dhidi ya Uhuru na Wenzake ihairishwe huku wegine wakidai mahakama hiyo ya ICC ni ya kisiasa na inaonea viongozi wa kiafrika.

Kuna baadhi ya wanasiasa ambao katika vikao vya hadhara na mikutano ya kisiasa wakilalama kuwa mahakama hiyo ya ICC na mahakama ya kisiasa yenye lengo la kubana nchi za kiafrika.