Wapiganaji Mali wasonga mbele

Imebadilishwa: 31 Machi, 2012 - Saa 14:43 GMT

Wapiganaji wa Mali wa kabila la Tuareg, wamesonga kusini hadi mji muhimu wa Gao, na wakaazi wa huko wanasema wamesikia risasi nyingi.

Kiongozi wa kijeshi Mali, Amadou Sanogo akizungumza Ijumaa

Wakuu wa huko wanasema Watuareg waliingia kwa magari yaliyokuwa na silaha nyingi.

Ijumaa, kiongozi wa waasi jeshini waliopindua serikali ya Mali juma lilopita, waliomba msaada wa kimataifa kupambana na wapiganaji.

Ujumbe wa viongozi wa jeshi, umekwenda nchi ya jirani ya Burkina Faso, kuzungumza na Rais Blaise Compaore, ambaye anapatanisha katika msukosuko huo.

Mashambulio ya wapiganaji yameshika kasi katika eneo kubwa la jangwa, kaskazini mwa Mali.

Sasa wameuteka mji wa Gao, ambao una kikosi kikubwa kabisa cha jeshi kaskazini.

Shambulio hilo limetokea siku moja tu baada ya wapiganaji hao wanaoongozwa na kabila la Tuareg na wapiganaji wa Kiislamu, kuuteka mji mwengine muhimu, mji wa Kidal.

Makundi hayo mawili yamekuwa yakipigana bega kwa bega, lakini haijulikani vipi watagawana madaraka.

Wapiganaji wa kundi la MNLA wanataka kulitenga eneo la kaskazini, wakati kikundi cha Waislamu, kiitwacho Ansar Edine, kinataka kuleta sheria za Kiislamu.

Huku nyuma, serikali ya kijeshi ya Mali, imetuma ujumbe Ouagadougou, mji mkuu wa nchi jirani ya Burkina Faso, kufanya mazungumzo na Rais Blaise Campaore, siku mbili kabla ya mataifa ya Afrika Magharibi kuanzisha vikwazo vikali dhidi ya Mali.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.