Waasi wa Columbia waachilia mateka

Waasi wa kundi la Farc nchini Columbia wamewaachia huru mateka kumi waliokuwa wamezuiliwa kwa zaidi ya miaka kumi.

Mateka hao wakiwa ni maafisa wa polisi na wanajeshi walichukuliwa na ndege ya kijeshi kutoka Brazil kutoka msitu mmoja na kupelekwa hadi mjini Villavicencio ambapo walifanyiwa uchunguzi wa kiafya kabla kupokewa na jamaa na marafiki zao.

Image caption Mateka wako huru baada ya kuzuiliwa kwa miaka 10

Mateka hao baadaye walipelekwa mjini Bogota.

Rais wa Columbia Juan Manuel Santos amekaribisha hatua hiyo ya waasi wa Farc lakini ameongeza kuwa haitoshi.

Watu hao walitekwa katika uwanja wa mapambano kati ya vikosi vya usalama vya Columbia na waasi hao wa Farc, miaka kumi iliopita.

Punde tu walipowasili, filamu za mateka hao wakiwa na furaha zilionyeshwa kwenye televisheni ya kitaifa wengine wakipeperusa bendera ya nchi yao.

"Karibuni wanajeshi na polisi wa Columbia, uhuru wenu umechelewa lakini sasa fursa ni yenu kujivunia" alisema Rais Santos.

Hata hivyo Rais Santos amesisitiza kuwa waasi wa Farc sharti waache kuteka nyara raia wa kawaida na kuwa lazima mamia waliosalia chini ya udhibiti wao waachiwe huru pia.

Juhudi zilizochangia mateka hao kuachiwa huru zilisimamiwa na shirika la kimataifa la msalaba mwekundu, kundi la wazee kutoka Columbia na aliyekuwa seneta Piedad Cordoba.