Bingu wa Mutharika hali mahututi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bingu wa Mutharika

Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika amelazwa hospitalini baada ya kupatwa na mshutuko wa moyo.Duru zinasema kiongozi huyo yuko hali mahututi katika hopsitali moja mjini Lilongwe baada ya kuanguka asubuhi.

Mkewe Callista Mutharika pamoja na kakake Peter Mutharika walimtembelea kiongozi huyo hospitalini.Japo haijathibitishwa rasmi ikiwa hali ya afya ya rais huyo inamuzuia kuongoza nchi, katiba ya taifa inampa uwezo Makamu wa Rais kuongoza endapo rais ameondoka madarakani kwa namna moja au nyingine.

Mwandishi wa BBC mjini Blantyre amesema ikiwa Makamu wa Rais Joyce Banda atafanywa kaimu rais , itakuwa mageuzi makubwa katika uwongozi nchini humo.

Bingu wa Mutharika alimtimua chamani Makamu wake Joyce Banda japo hangeweza kumuondoa kama Naibu Rais wake. Chama tawala DPP kimemteuwa kakake rais, Peter Mutharika ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje kuwa mgombea wake wa urais.Bingu wa Mutharika aliingia madarakani mwaka wa 2004 na kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka wa 2009.

Katika siku za karibuni utawala wake umekosolewa vikali ndani na nje ya Malawi.Mwaka jana Wa-Mutharika alimfukuza balozi wa Uingereza, Fergus Cochrane-Dyet, baada ya nyaraka za siri kumnukuu balozi huyo akisema Rais wa Malawi alipinga kukosolewa. Uingereza ilijibu kwa kumtimua balozi wa Malawi mjini London na kusimamisha msaada.