Tume ya Katiba Mpya yatangazwa Tanzania

Image caption Rais wa Tanzania Jakaya Kiwete atangaza Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete leo ametangaza tume ya itakayokusanya maoni ya Katiba Mpya nchini humo ambayo itaongozwa na Waziri mstaafu Joseph Warioba.

Ndani ya tume hiyo yapo majina maarufu ambayo ni pamoja na Jaji Mkuu mstaafu Agustino Ramadhani ambaye atakuwa Makamu mwenyekiti wa tume hiyo.

Wengine ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi huru za Afrika hivi sasa Umoja Afrika AU Dk. Salim Ahmed Salim ambaye ameteuliwa kuwa mmoja wa makamishna wa tume hiyo.

Wapo pia wanasheria maarufu wa Tanzania ambao wameteuliwa kuwa makamishna wa tume hiyo ambapo ni pamoja na Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Paramagamba Kabudi na Dk. Sengodo Mvungi Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo hapa.

Rais Kikwete ametangaza tume hiyo Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 iliyofanyiwa marekebisho baada ya kuzua mvutano bungeni hivi karibuni.

Kwa mujibu wa sheria hiyo Rais baada ya kualika majina kutoka makundi mbali mbali ya jamii anapaswa kushauriana na Rais wa Zanzibar wakati wa kufanya uteuzi huo.

Tayari Makundi mbali mbali ya jamii yalishawasilisha majina kwake mwezi uliopita kwa ajili ya uteuzi huo.

Kutangazwa kwa tume hiyo ina maana sasa mchakato wa kuandika katiba mpya nchini Tanzania umeanza na kilichobaki ni kuapishwa kwa tume hiyo ambapo wakati wowote itatangaza ratiba ya kuandika katiba mpya.