Traore aapishwa Rais wa Mpito Mali

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Traore baada ya kuapishwa Bamako

Dioncounda Traore ameapishwa kuwa Rais wa mpito wa Mali kuashiria kurejea kwa utawala wa kiraia baada ya mapinduzi kutokea mwezi uliopita nchini humo.

Serikali ya spika huyo wa zamani sasa ina siku 40 za kuandaa uchaguzi.

Waandishi wanasema muda huo huenda usitoshe kuandaa uchaguzi hasa kwa kuzingatia eneo la kaskazini kuwa mikononi mwa waasi.

Majukumu ya kiongozi wa mapinduzi Kepteni Amadou Sanogo hayajajulikana.

Bw Traore aliapishwa na Rais wa mahakama Kuu Nouhoum Tapily katika hafla fupi mjini Bamako.

Mataifa ya Afrika Magharibi yaliondoa vikwazo vyake kwa Mali baada ya Kepten Sanogo kukubali kuachia madaraka.

Kabla ya makubaliano yaliyofikiwa Ijumaa aliomba Jumuiya ya Ecowas kusadia kuwaondoa waasi wa Tuareg na wenzao wapiganaji wa Kiislam ambao wameliteka miji muhimu ya kaskazini.

Hata hivyo hata awali alishasema kuwa anachohitaji ni msaada wa vifaa na uratibu akipinga vikosi vya wanajeshi 3000 wa Ecowas kuingilia kati.

Pamoja na hayo Ecowas bado inatafakari uwezekano wa kupeleka vikosi na mawaziri wa mambo ya nje wanakutana Alhamis katika mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan kwa majadiliano.

'Hakuna msukumo'

Waandishi wanasema Bw Traore, mwenye miaka 70, amekuwa na nia ya kuwa Rais lakini amekuwa na matumaini ya kupata nafasi hiyo kupitia kura akigombea uchaguzi ambao ulipangwa kufanyika mwezi huu.

Mtaalam huyo wa Hisabati anaongoza chama kikubwa cha siasa Alliance for Democracy nchini Mali na alikuwa mshirika mkubwa wa Rais aliyepinduliwa Amadou Toumani Toure, ambaye alijiuzulu rasmi Jumapili.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa mpito Traore na Kepten Sanogo

Akifahamika kama ATT, Rais huyo wa zamani alitakiwa kuondoka madarakani baada ya miezi miwili akikamilisha muda wake na watu wamekatishwa tamaa na serikali yake kwa kutochukua hatua za kutosha kupambana na ufisadi na ukosefu wa ulinzi na hatimaye uasi katika eneo la kaskazini.

Matokeo yake watu wengi wana wasiwasi na Bw Traore, Mwandishi wa habari wa Bamako Martin Vogl alikiambia kipindi cha BBC Network Africa programme.

Bw Traore hachukuliwi kama kiangozi mwenye ushawishi wala wtu wengi hawamuonikamakiongozi kiasili, anasema.

Waandishi wanasema wakati kuapishwa kwa Bw Traore kunaweza kuleta matumaini, amani ya kudumu katika eneo la kaskazini haiwezi kupatikana mpaka hatima ya kisiasa ipatikane.

Kufuatia makubaliani ya Ecowas, Kepteni Sanogo aliiambia BBC kuhusu suala la kubadilishana madaraka kuwa: "Makubaliano yako wazi.[Traore] atakaa hapa kwa siku 40 na baada ya siku 40 kamati yangu na Ecowas tutakaa pamoja kutengeneza vyombo vya mpito."

Alipoulizwa iwapo kwa maneno hayo atarejea tena madarakani baada ya muda huo alijibu: "Sikusema hivyo.Sijui."

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeonya kuwepo janga la kibinadamu baada ya mapigano ya kaskazini.

Waasi wa Tuareg, wanaoishi katika Jangwa la Sahara nchiniMalina nchi nyingine jirani kwa miaka mingi wanadai wamekuwa wakipuuzwa na uongoziBamako.