Wasifu: Traore alikuwa na ndoto ya Urais

Haki miliki ya picha
Image caption Traero, Rais wa mpito Mali

Ilikua ni ndoto yake Dioncounda Traore kuwa siku moja angechaguliwa kwa kura kuwa Rais wa Mali katika uchaguzi huru na wa haki;lakini hatimaye hata kama si moja kwa moja ni mapinduzi ndiyo yaliyomuwezesha kuwa kiongozi wa nchi hiyo.

Ajabu ya mambo ni kwamba njama ya mapinduzi ya March 22 ilipangwa katika mji wa kambi ya kijeshi wa Kati, ambako ndiko Dioncounda Traoré alikozaliwa mnamo mwaka 1942.

Alisomea nchini Ufaransa ambako baadaye alijipatia shahada ya uzamifu katika hisabati.

Aliporejea nchini Mali alifanya kazi hadi kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa shule ya ya taifa ya uhandisi katika mji mkuu Bamako.

Baadae alihusika na siasa na kuwa mwaanzilishi wa muungano wa demokrasia nchini Mali.

Chama ambacho kilimsukuma Alpha Konare, kuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini mnamo 1992.

Baada ya hapo Bwana Traore alishikilia nyadhifa mbali mbali zikiwemo wizara za ulinzi na mambo ya nje.

Anaunga mkono mapendekezo ya kuwa na sheria ya familia ambayo inawapa haki sawa wanawake na wanaume.

Sheria hiyo imezusha malalamiko nchini Mali pale mashirika ya kiislamu yalipoipinga miaka mitatu iliyopita.

Lakini changamoto kubwa ni kurudisha utulivu na umoja kwa nchi ya Mali baada ya kurithi nchi iliyogawanyika kutokana na uasi wa kaskazini.