Zuma aowa tena

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ametangaza kwamba atafunga ndoa ya sita juma lijalo.

Haki miliki ya picha AFP

Rais huyo mwenye umri wa miaka 70, atamuoa mchumba ake kwenye harusi ya kijadi huko Kwa Zulu Natal.

Gloria Bongekile Ngema, mfanya biashara kutoka Durban, ameshaonekana mara nyingi akifuatana na rais lakini kutoka juma lijalo, wawili hao watakuwa wameowana rasmi kijadi.

Harusi inatarajiwa kuwa ya fahari lakini ya faragha katika kijiji cha Nkandla, katika jimbo la Kwa Zulu Natal, nyumbani kwao Rais Zuma.

Rais Zuma ni mtu anayefuata mila za kabila lake la Zulu.

Mwenyewe amezaliwa na baba aliyekuwa na wake kadha.

Na ndoa yake kwa Bi Ngema ni ya sita, ingawa kutoka juma lijalo atakuwa na wake wane tu.

Mmoja, ambaye ni waziri wa serikali, alimuacha.

Na mwengine alijiiuwa.

Nyumba ya Rais Zuma imetengenezwa sana ili kuweza kuweka familia yake.

Inafikiriwa ana watoto 20.

Lakini hivi karibuni alisema ndoa ya juma lijalo ndio itakuwa ya mwisho.