Wanamapinduzi G.Bissau kuunda serikali

Haki miliki ya picha INTERNET
Image caption wanajeshi waliopindua serikali G Bissau

Wanajeshi waliotwaa madaraka wiki jana huko Guinea Bissau wameunda baraza la mpito kusimamia taifa hilo la Afrika Magharibi. Baraza jipya linashirikisha makundi ya upinzani. Hii inajiri wakati ujumbe wa kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS unazuru nchini humo kujaribu kushawishi watawala wapya kurejesha utawala wa kiraia.

Wanajeshi walipindua serikali ya mpito Alhamisi ya wiki jana wakilalamikia mpango wa kupunguza idadi yao. Hakuna rais aliyemaliza mhula wake nchini Guinea Bissau, tangu nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1974 kutoka kwa Ureno.

Mapinduzi ya sasa yamefanyika kabla ya raundi ya pili ya uchaguzi wa urais uliofanywa kufuatia kifo cha rais Malam Bacai Sanha. Mmoja wa wagombea wakuu ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani Carlos Gomes Junior amekamatwa na wanajeshi pamoja na rais wa mpito Raimundo Pereira.

Vyama 22 kati ya 35 vinashiriki kwenye baraza jipya la mpito.Hata hivyo, chama cha bw Carlos cha 'Independence of Guinea-Bissau and Cape Verde' (PAIGC), haikishirikishwi. Manowari za Ureno na ndege ya kijeshi imetumwa Guinea Bissau kusaidia kuhamisha raia wanaoishi nchini humo.Haijabainika kundi au mtu aliyechochea mapinduzi ya sasa ambayo wadadisi wanasema haihusishi wakuu wa jeshi.