Mkenya atuzwa kwa kutetea mazingira

Image caption Ikal Angelei

Ni kutokana na harakati zake kutetea mazingira ambapo Ikal Angelei amepata tuzo ya mwaka huu ya Goldman inayotuzwa raia wanaotetea utunzi wa mazingira katika maeneo ya mashinani.Bi Angelei anaendesha shughuli zake katika eneo la Turkana, Kaskazini mwa Kenya ambalo hupakana na nchi za Ethiopia, Sudan Kusini na Uganda.Juhudi zake zimemfanya kuwa mshindi wa dola laki moja unusu ambazo huandamana na tuzo ya Goldman.

Binti huyu amepinga mpango wa ujenzi wa bwawa kubwa zaidi barani Afrika GIBE-3. Bwawa hili ni mradi wa serikali ya Ethiopia kuisaidia kuzalisha umeme wa kutumiwa ndani ya nchi na pia kuuza nje.Ikal Angelei anapinga ujenzi wa bwawa hili akisisitiza linatishia kukausha ziwa Turkana ambalo huwa tegemeo la jamii kutoka nchi tatu zinazotegemea maji hayo.

Serikali ya Ethiopia imeanza ujenzi wa bwawa kubwa GIBE-3 ambalo linatoa maji yake kwa mto Omo, ambao hupata 80% ya maji yake kutoka ziwa Turkana.Waziri Mkuu Meles Zenawi ameapa kuendelea na ujenzi wa bwawa la GIBE-3 akisisitiza utasaidia katika kilimo cha nyunyiziaji waji kwenye bonde la mto Omo sawa na kutoa umeme kwa nchi.Serikali ya Kenya ambayo inatarajiwa kuwa mteja wa umeme huo imeunga mkono mradi huu.

Ikal Angelei amehofia kwamba bwawa hili litaangamiza maisha ya maelfu ya jamii zinazoishi katika bonde la mto Omo pamoja na wanaotegemea ziwa Turkana.Amesema jamii hususan wafugaji watalazima kuhamia maeneo ya malisho ikiwa ziwa litakauka. Hii huenda ikachochea makabiliano zaidi dhidi ya malisho na maji baina ya jamii za wafugaji.

Mwaka jana kulitokea ghasia kati ya jamii ya Turkana kutoka Kenya na Merille kutoka Ethiopia dhidi ya malisho na maji.