Mmsionari mwanamke atekwa nyara Mali

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waasi wa Tuareg

Raia wa Uswizi ametekwa nyara katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Timbuktu Kaskazini mwa Mali. Maafisa na wakaazi wamemtaja raia huyo kama Beatrice ambaye pia ni mmisionari.

Wanasema alichukuliwa na watu waliojihami kutoka kwa makaazi yake. Raia wengi wa kigeni walihama Timbuktu baada ya waasi wa Tuareg na wale wa kiisilamu kuudhibiti mji.Utakeji nyara huu unajiri kukiwa na hofu kwamba eneo hilo huenda likatumika kama ngome ya mtandao wa Al-Qaeda ambalo huendesha harakati nchini humo.

Tawi la Al Qaeda Afrika Kaskazini{Aqim},linawashikilia raia 13 wa kigeni.Afisa mmoja wa Timbuktu Mohamed Ould Hassen amenukuliwa akisema Beatrice alichukuliwa na watu sita waliokuwa na silaha.

Wakaazi wanasema mama huyo ameishi Timbuktu kwa miaka mingi na huzungumza lugha asilia za eneo hilo.Kundi la kiisilamu Ansar Dine pamoja na lile na Tuareg lilitwaa eneo nzima la Kaskazini mwa Mali baada ya serikali kupinduliwa na jeshi.