Kanda ya ubakaji yazua ghadhabu A. Kusini

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wanaopinga kitendo cha ubakaji

Watu nchini Afrika Kusini wameelezea ghadhabu baada ya kusambazwa kwa kanda ya video ikionyesha msichana mmoja akibakwa na kundi la wanaume.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 17, na anayearifiwa kuwa na akili tahira inayomfanya kuwa kama mtoto mwenye umri wa miaka mitano, alibakwa katika mtaa wa Soweto.

Kanda hiyo inayoonyesha wanaume hao wakicheka wakati wakifanya kitendo hicho, imesambazwa kupitia Internet na hata simu za mkononi. Polisi wamempata msichana huyo na kuwakamata watu wanane kwa makosa ya utekaji nyara na ubakaji.

Msichana huyo alitoweka mwezi Machi hali yake ikiwa haijulikani hadi waandishi wa gazeti la Daily Sun walipotoa kanda hiyo kwa polisi.

Taarifa ya agazeti hilo imeelezea kuwa kanda hiyo ni ya dakika kumi na kwamba msichana huyo anasikika akipiga mayowe.

Maafisa wa utawala wameonya yeyeyote aliye na kanda hiyo kuifuta au huenda akakamatwa na kushtakiwa kulingana na sheria ya dhulma za za kimapenzi nchini humo.

Waziri wa mambo ya wanawake na watoto nchini humo, Lulu Xingwana, alinukuliwa akisema " pamoja na uchungu aliopitia msichana huyo sasa analazimika kukabiliana na aibu nyingine kwa hadhi yake"

Tukio hilo limeangazia wazi swala la ubakaji nchini Afrika. Utafiti wa hivi karibuni umeelezea kuwa zaidi ya robo ya wanaume nchini humo wamekiri kufanya kitendo cha ubakaji.

Takriban visa 66,000 vya ubakaji viliripotiwa nchini humo mwaka jana ingawa wataalamu wansema kuwa waathirika hulazimika kukaa kimya.