Mpango wa amani Syria waporomoka

Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia wa Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema Syria imeshindwa kutekeleza mpango wa amani uliotaka majeshi ya serikali na silaha kuondolewa maeneo ya makaazi.

Katika waraka wake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ki-moon pia ametaka kundi la waangalizi walioko ndani ya nchi hiyo kuongezwa hadi 300.

Habari kutoka Syria zinasema ghasia zimeendelea na kutishia majaaliwa ya mpango wa amani ambao ulianza wiki jana.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton anakutana na mawaziri wenzake katika mkutano mjini Paris Ufaransa kujadili mzozo wa Syria.

Mpango wa amani wa Syria ulipendekezwa na Mujumbe wa Kimataifa Koffi Annan kama hatua ya kumaliza machafuko ya zaidi ya mwaka mmoja ambapo takriban watu 9000 wamekufa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana baadaye Alhamisi kujadili ripoti mpya ya kupanua waangalizi wake ndani ya Syria.

Hata hivyo azimio lolote linatarajiwa kutangazwa wiki ijayo.

Huku haya yakiarifiwa rubaa kutoka Uturuki zinaarifu maafisa wa bandari kuu wanakagua meli moja inayodaiwa kusheheni silaha zikielekea Syria.