Amadou Toure akimbilia Senegal

Image caption Amadou Toure

Kiongozi wa Mali aliyeondolewa madarakani mwezi jana Amadou Toumani Toure amekimbia kupata hifadhi katika nchi jirani ya Senegal, licha ya wandani wake kuachiwa huru.

Bw. Toure aliwasili nchini Senegal akiandamana na familia yake. Mwandishi wa BBC amesema kiongozi huyo amekuwa katika ubalozi wa Senegal nchini Mali tangu kutokea mapinduzi hayo.

Wadadisi wamesema hatua ya Toure kutafuta hifadhi ni ishara ya kuvunja moyo baada yake kusifiwa kama mojawapo wa viongozi waliotetea utawala bora barani Afrika.

Kiongozi huyo alipongezwa pale aliporejesha utawala wa kiraia mwaka wa 1992 kufuatia mapinduzi ya kijeshi.

Mwongo mmoja baadaye alichaguliwa na raia kwa imani ya kutetea demokrasia.

Mwandishi wa BBC mjini Bamako amesema Toumani Toure aliamua kuondoka Mali kuepuka ghathabu ya wanajeshi waliokuwa wakitishia kumkamata.

Wanajeshi wa Mali waliendesha mapinduzi kulalamikia ulegevu wa serikali katika kukabiliana na maasi kaskazini mwa nchi.

Tangu kutokea mapinduzi hayo, waasi wa Tuareg na makundi ya kisiilamu yameyateka maeneo mengi kaskazini mwa Mali.