Majeshi Mali yaachiliwa wanasiasa wote

Jeshi la Mali limewaachilia huru maafisa wote wa kisiasa na kijeshi waliokamatwa mapema wiki hii, hiyo ni taarifa kwa mujibu wa viongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita.

Image caption Aliyekuwa Rais,Toumani Toure aelekea Senegal

Katika taarifa nyingine, nchi jirani ya Senegal imesema rais wa zamani wa Mali aliyeondolewa madarakani, Amadou Toumani Toure, alikuwa amepanda ndege kuelekea Dakar mji mkuu wa Senegal.

Senegal imeeleza wiki hii kuwa Toure alikuwa amepata hifadhi katika ubalozi wake mjini Bamako.

Toure aliondoka katika makaazi yake Marchi 22.

Kukamatwa kwa maafisa 22 kulikofanywa na vikosi vya usalama, kulisababisha shutuma za kimataifa kutokana na kitendo hicho siku chache baada ya utawala huo wa kijeshi kujiondoa kumpisha kiongozi wa kiraia.

Hatua ya Mali kuchelewa kurejea katika utawala wa katiba, kutahatarisha juhudi za majirani zake kuisaidia nchi hiyo kuyatwaa tena maeneo yake ya kaskazini yaliyokaliwa na waasi tangu mapinduzi ya kijeshi nchini humo.

Habari kutoka wizara ya ulinzi ya Mali zimethibitisha kuwa maafisa 11 wa kiraia na wale wa kijeshi ambao walikuwa wakishikiliwa katika mji wa kijeshi wa Kati, kaskazini mwa mji mkuu Bamako, wameachiliwa.

Kuachiliwa kwa maafisa hao kulithibitishwa baadaye katika taarifa fupi iliyotumwa na watawala wa kijeshi kwa njia ya barua pepe.

Maafisa wote waliokuwa wamekamatwa walionekana kuwa watu wa karibu na Bwana Toure, ambaye alitarajiwa kujiuzulu kabla ya uchaguzi wa April 29.

Mashirika ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, Jumatano wiki hii walishutumu vikali kukamatwa kwa maafisa hao.

Wanasiasa wamelilaumu jeshi kwa kutotaka kuachia madaraka.