ECOWAS kutuma jeshi Mali na G.Bissau

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Viongozi wa Ecowas

Viongozi wa kanda ya Afrika Magharibi wameafikiana kutuma wanajeshi katika nchi za Mali na Guinea-Bissau kufuatia mapinduzi katika hizo. Nchi wanachama wa ECOWAS zilitoa taarifa ya pamoja baada ya kufanya kikao cha dharura ambapo wanajeshi kati ya 500 na 600 watatumwa Guinea-Bissau.

Wanajeshi wengine 3,000 wataelekea Mali kusaidia kipindi cha mpito pamoja na kuyakomboa maeneo ya kaskazini ,yanayodhibitiwa na waasi wa Kiisilamu na Tuareg. Mwandishi wa BBC mjini Abidjan amesema hakuna ratiba rasmi kupeleka kikosi huko Mali hadi pale utawala wa mpito utakapo toa ratiba yake ya jinsi itakavyoshirikiana na wanajeshi wa ECOWAS.

Kuhusu hali ya Guinea-Bissau, wanamapinduzi wamepewa siku tatu kurejesha utawala wa kiraia la sivyo wakabiliwe na vikwazo.Kikosi kinachotumwa Guinea-Bissau kitasaidia kuweka usalama wakati nchi hiyo ikrejelea utawala wa kiraia.

Wanajeshi waliopindua serikali ya Bissau walipinga mpango wa Waziri Mkuu Carlos Gomes kupunguza idadi ya wanajeshi hao.Kaimu Rais Raimundo Pereira na Bw. Gomes walikamatwa wakati wa mapinduzi.

Guinea-Bissau imekuwa kivukishio cha mihadarati kutoka Amerika Kusini kuingia Ulaya. Hakuna Rais aliyemaliza mhula tangu taifa hilo kupata uhuru wake kutoka kwa Ureno.